Monday, December 24, 2012

Uwanja wa ndege Mwanza na mikosi


UWANJA WAAA NDEGE wa Mwanza, unapanuliwa  uweze kufikia viwango vya kimataifa,ili kuweza kuhudumia nchi zote za Maziwa Makuu.
Njia ya kurukia inapanuliwa ili kuwezesha ndege kubwa kuuruka na kutua,bila matatizo,na mnara wa kuongozea ndege unawekewa vifaa vya kisasa.
 Miaka michache iliyopita,uwanja huu umekuwa gomzo kwa ajali za ndege,na ni mahali ambapo ndege ya kwanza ilitekwa hapa Tanzania.
Siku moja, saa 10:15 hivi  jioni, ndege ndogo, F06  Cessna iliyokuwa na marubani wawili, iliparamia mlima; ikaugonga na kuwaka moto, dakika chache tu baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza.
  Ndege hiyo ya Shirika la Auric Air Services, yenye uwezo wa kubeba abiria kama wanane, ilianguka na kuwaka moto; ikasababisha watu wawili ambao ni marubani, Chris Marley mwenye uraia wa Uingereza na Mathew Smith, Mwanaanga wa Australia kufariki dunia.
   Ndege hiyo ilidaiwa kutengenezwa Marekani miaka michache iliyopita, na ilikuwa ikikodishwa migodini na kusafirisha watalii.
 Ajali iliyotokea ilitokana na kugonga mlima ulioko jirani na uwanja wa ndege wa Mwanza, marubani hao walipokuwa wakifanya mazoezi.
  Ilipoparamia mlima, ikaanguka na kuanza kuwaka moto, kitendo kilichofanya maofisa wa uwanja wa ndege na maofisa wa Jeshi la wananchi(JWTZ) kwenda kuzima moto huo na kujaribu kufanya uokozi.
   Hii ni ajali  kama ya sita katika uwanja huo katika muda usiozidi miaka 10.
Uwanja wa ndege wa Mwanza ni muhimu sana katika nchi za Maziwa     Makuu, lakini unaandamwa na mikosi ya kila mara.
    Licha ya kuwa kandoni mwa Ziwa kubwa kuliko yote Afrika, Ziwa Victoria , au kuwa jirani na Rwanda , Uganda , Burundi , Kenya na Jamhuri ya Congo(DRC); uwanja wa ndege wa Mwanza, upo maeneo yanayozalisha pamba, kahawa, samaki, dhahabu, almasi na mbuga za wanyama maarufu sana Duniani; Serengeti.Mbuga za Serengeti ziko kilomita 100 tu kutoka Mwanza.
    Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege nchini(TAA), Prosper Tesha, aliwahi kusema kuwa sasa uwanja huo utafanyiwa matengenezo ili kuboresha miundombinu yake.
     Mwaka 2003 uwanja huo ulisafirisha jumla ya abiria 5,344 tu wa kimataifa;wakati abiria wa ndani walioutumia uwanja huo hawakuzidi 125,499 kwa sababu anuwai, ukiwemo uduni wa usalama na miundombinu.
    Minofu ya sangara iliyosafirishwa mwaka huo kutoka katika viwanda vya kusindika minofu ilikuwa tani 13,426.
    Kulingana na rekodi za habari za viwanja vya ndege duniani, uwanja huo umegubikwa na ‘mikosi’ ama ‘pepo wachafu’ kufuatia ndege kama sita sasa kuanguka uwanjani hapo.
 Ukiacha ajali hiyo ya Alhamisi, Aprili 3,Ajari  nyingine ni ya Machi 24 mwaka 2005 wakati Ilyushin 76 ya mizigo ya Shirika la Air Trans Inc. la Moldova , Ukraine , ilipoanguka Ziwani na kuua  wafanyakazi saba na rubani, wote raia wa iliyokuwa Jamhuri ya Urusi , USSR .
    Ilikuwa ikiruka kutoka uwanjani hapo, ikiwa na tani 50 za minofu ya sangara kutoka viwanda vya kusindika samaki vya jijini Mwanza; na ilikuwa safarini kwenda Croatia kupitia Benghazi na Osijek .
     Hata hivyo, mkosi wa kwanza uwanjani hapo ulitokea Feburuari 26 mwaka 1982, siku ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania(ATC), Boeing 737 ‘Tango Charlie 207’ iliyokuwa na jina Kilimanjaro mbavuni, ilipotekwa nyara na kulazimishwa kwenda London.
   Ilikuwa na abiria 74 na wafanyakazi watano; ikiendeshwa na Kapteni Deo Mazula, wakati Yassin Membar(21), Mohamed Tahir Ahmed(21),Abdallah Ali Abdallah(22), Mohamed Ali Abdallah(26) na kiongozi wao Musa Membar(25) walipoiteka nyara ndege hiyo na kuunajisi uwanja huo kwa mara ya kwanza kabisa.
    Walikuwa na silaha ‘mwanasesere,’ kufuatia usalama dhalili uwanjani hapo, wakazipenyeza ndegeni, ambamo baada ya kuwatisha abiria na wafanyakazi wa ndege, walipata ‘Revolver’ katika chumba cha rubani.
   Pia, walipata bastola nyingine yenye risasi, baada ya kuwapekua abiria. Tena, walipata Shotgun mbili zisizokuwa na risasi, mali ya abiria ambazo hazikuwa zimehifadhiwa vizuri.
      Ndege hiyo ilirejeshwa nchini na abiria wake 74 Machi 4 mwaka huo wa 1982 wakapokelewa kishujaa, wakati Membar na wenzake walifungwa jela kati ya miaka minane na mitatu kwa makosa hayo ya kigaidi.
   Oktoba Pili, mwaka 2001 ndege nyingine yenye shehena ya silaha, ikazuiliwa uwanjani hapo kwa saa 30; ikajakuachiliwa baadaye kwa maagizo ya kiusalama kutoka Dar es salaam.
    Ndege hiyo ilitokea Batislava, Jamhuri ya Slovak; ikipitia Israeli hadi Misri, kabla ya kutua jijini Mwanza.
   Mkuu wa Mkoa, Stephen Mashishanga, wakati huo akasema mwanzoni walidhani vifaa, kumbe zilikuwa silaha zilizokuwa zikienda nchi zenye migogoro.
    ‘Laana’ hiyo ilitua Bungeni baadaye, Mbunge wa Shinyanga mjini, Leonard Derefa, akamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ajiuzulu.
    Laana hiyo ikaongezwa na Mtunzi wa Filamu ya Mapanki(The Darwin’s Nightmare), Hubert Sauper, aliyeutangazia Ulimwengu kwamba, ndege zinazofika Mwanza kuchukua minofu ya sangara, huja na shehena ya silaha zinazorutubisha vita na machafuko nchi za Maziwa Makuu.
     Mfaransa huyo,akasema kupitia filamu hiyo iliyorushwa Dunia nzima, kwamba madege yanayotua Mwanza huja na bunduki kabla ya kupakia samaki; yaani hubadilisha samaki kwa silaha-“Guns For Fish”!
    Watu waliohojiwa na mtunzi huyo wa filamu ya tashtiti walidai, madege, Ilyushin-76, Boeing 707 na DC8 yaliyokuwa yakija Mwanza kuchukua samaki, yalikuwa yakishusha silaha katika nchi za migogoro, kabla ya kupakia samaki Mwanza.
    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini(TAA), Prosper Tesha, alikanusha madai ya filamu hiyo ya kizandiki, akasema mambo yalikuwa shwari uwanjani hapo, kulingana na viwango vya kimataifa vilivyowekwa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani, ICAO.
  Hata hivyo, wakazi wa jiji la Mwanza waliofanya mahojiano na mwandishi wa makala hii, mwishoni mwa wiki, walishauri matengenezo yatakayofanwa yaende sambamba na uboreshaji wa ulinzi na miundombinu itakayoepusha ajali, ili kuondoa mikosi inayouandama uwanja huo.
    Miundombinu inayoshauriwa kuimarishwa ni pamoja na vifaa vya uchunguzi mkali, security check point  na mitambo maalum yenye kubaini silaha na mabomu, metal detector.
 Sauper, alidai, wakati akipiga picha za filamu yake kwamba, alipenya uwanjani hapo kwa kuwahonga baadhi ya watu hadi akafanikiwa kupiga picha katika chumba cha kuongozea ndege, traffic control tower, ambako mwangoza ndege mmoja alipigwa picha akiacha kuongoza ndege na kuanza kuwaua nyuki waliokuwa wakirandaranda katika vioo vya madirisha!
    Wamesema, kama Mwanza ni kitovu cha Biashara kama vilivyo viwanja kama John F. Kennedy International, New York city na Newark(New Jersey), Sauper asingepata upenyo wa kupigapiga picha hata maeneo ya kijeshi na kuonyesha mabaki ya ndege zilizokwisha anguka uwanjani hapo.
    “Je, viwanja vikubwa kama Mirabel , Canada , Honolulu , Charles De Gaulle, Fiumicino, Palma de Majorca n.k wanaruhusu watu kama Sauper kupiga mapicha ovyo na kudhalilisha  ?” wananchi hao waliozungumza na  Mtanzania Jumapili  wamehoji.
   Ajali ya Alhamisi ya ndege hiyo, Cessna, iliyoua watu wawili ni mfuatano wa majanga mengine yasiyopungua saba katika uwanja huo tangu mwaka 2000.
Ajali nyingine iliyohusisha ndege za aina hii duniani, ni ile ya Septemba 25, mwaka 1978, ambapo Cessna 172 iligongana na Boeing 727 angani huko San Diego na kuua watu 150.
   Kulingana na matukio haya, baadhi ya wananchi hapa wanadhani uwanja wa ndege wa Mwanza kuna mikosi ama ‘bundi’ wanaofanya ughubikwe na ajali za kila mara ama matukio ya kupakwa matope. Katika Filamu ya Darwin’s Nightmare, iliyozua mtafaruku hapa nchini, mabaki ya baadhi ya ndege zilizowahi kuanguka uwanjani hapo yanaonekana.
 Hata ajali ya miaka michache iliyopita, mabaki ya ndege hii ya Cessna  huenda yakahifadhiwa uwanjani hapo, kitu kinachofanya baadhi ya watu kuhofu kwamba wasafiri wanaweza kudhani uwanja huo si salama na ni eneo la ukanda wa ajali za ndege, kwa sababu kila afikaye uwanjani hapo, lazima ataona mabaki ya ndege zilizowahi kuanguka jirani na uwanja huo.
Hata hivyo, sasa serikali inauboresha uwanja huo kwa kupanua njia ya kurukia,running way, majengo ya ofisi na miundo mbinu mingine.
Hivi sasa,uwanja huo huhudumia ndege za ATCL,Precision,54O,Kenya Airways n.k
Mwanzaoni uwanja huu ulijengwa ili kuhudumia ndege za kijeshi,ukapanuliwa hata kuwa wa ndege za abiria na mizigo kama sangara, na husafirisha pia madini na mizigo mingine
                 Mwisho.





No comments:

Post a Comment